Diego Costa, mshambuliaji wa kihispania mwenye asili ya Brazil ambaye ameiongoza Chelsea kutwaa mataji matatu ndani ya misimu mitatu, mawili yakiwa ya ligi kuu.
Mshambuliaji huyo katika msimu ulioisha akiwa chini ya kocha Antonio Conte aliiongoza Chelsea kutwaa taji la ligi kuu huku yeye akiwa ndiye mchezaji aliyeifungia magoli mengi na mchezaji pekee aliyefunga magoli yaliyoipa klabu yake alama nyingi. Kwa magoli yake aliihakikishia Chelsea alama 15.
Lakini mwezi wa Juni baada ya msimu kuisha, mhispania huyo alipokea ujumbe wa simu aliotumiwa na kocha Antonio Conte akiambiwa hayupo kwenye mipango ya kocha huyo.
Naye kwa muda kidogo alishawai kukaririwa akisema ameshachoshwa na maisha ya Uingereza akivilalamikia vyombo vya habari nchini humo akisema vinambana sana. Alisema angependa kama angerudi Hispania katika klabu ya Atletico Madrid.
Na kweli kocha Antonio Conte alionesha kwamba kweli hana mipango nae, akaamua kumsajili mshambuliaji Alvaro Morata ili kuja kuziba pengo la Costa, lakini kama hiyo haitoshi akamuacha katima timu iliyosafiri mpaka barani Asia kufanya ziara yake huko kwa kucheza michezo ya kirafiki.
Naye Diego Costa alisafiri mpaka nchini Brazil ambapo huko amekuwa akifanya mazoezi mwenyewe. Lakini siku moja akiwa nchini humo alionekana kuchochea uhamisho wake wa kuondoka klabuni Chelsea mara baada ya kupiga picha akiwa na jezi ya Atletico Madrid, klabu ambayo imefungiwa kufanya usajili mpaka mwezi januari.
Licha ya Atletico Madrid kufungiwa kusajili mchezaji huyo amegoma kwenda timu nyengine kucheza kwa mkopo mpaka pale itakapofunguliwa kifungo hicho naye ikasemekana yupo tayari kukaa nje ya uwanja mpaka klabu hiyo itakapofunguliwa.
Lakini bila shaka kama akichagua kukaa nje basi bila shaka nafasi ya kucheza katika michuano ya kombe la dunia mwaka ujao itakuwa ni ndogo kwa vile ni ngumu kuitwa kama hajacheza mchezo wa ushindani.
Kocha wa Atletico Madrid, Diego Simeone alikaririwa akisema "kwa sasa nawatazama wachezaji waliopo klabuni, na bado wanasema wanataka kuendelea kubaki, wanataka kufunga magoli zaidi na kupambana kwa ajili ya mataji. Kuhusu Diego Costa labda tusubiri mpaka mwezi januari" akimaanisha kwa sasa anapambana kuwa sawa na wachezaji wake aliokuwa nao kwenye timu, kuhusu Diego Costa haiwezekani kumchukua mpaka kifungo chao kitakapoisha.
Sasa swali lililopo, je mchezaji huyo ataendelea kubaki Chelsea ili acheze kwa ajili ya kombe la dunia au ataendelea kuwa nje mpaka Atletico Madrid itakapotolewa kifungoni?
No comments:
Post a Comment